Fastjet yashiriki mashindano ya Sports Xtra Bonanza 2018

Bill Marwa @BillMarwa

Ni shamra shamra ndani ya viwanja vya Leaders jijini Dar es salaam. Timu ya mpira wa miguu ya fastjet imejinoa tayari kwa mashambulizi dhidi ya timu pinzani katika mashindano ya Sports Xtra Bonanza yaliyofanyika siku ya mei mosi.

Fastjet inaanza kwa kasi kwa ushindi wa mechi yake ya kwanza ambapo inaibuka kidedea kwa kuitandika timu ya shirika la viwango Tanzania TBS bao moja kwa bila. Aidha timu ya fastjet inatoa sare mechi mbili zinazofuata na kushindwa kuendelea katika hatua zinazofuata kwa tofauti ya magoli. 

“Tunajivunia kwa kuwa timu yetu ilicheza vizuri, tumepungukiwa pointi kuibuka washindi wa jumla lakini tumekuwa washindani wazuri.” Alisema Lucy Mbogoro, msemaji wa fastjet aliyekuwa uwanjani hapo. 

“Mashindano haya ni mazuri sana kwa fastjet kwa kuwa yanatukutanisha na wateja wetu na kutuwezesha kutoa huduma mbalimbali hapa uwanjani ikiwemo mauzo ya tiketi, kujibu maswali ya wateja wetu na kupata fursa ya kutatua changamoto zao mbalimbali.” Aliongeza. 

Aidha mashindano haya yanawakutanisha wafanyakazi wa timu za makampuni mbalimbali pamoja na mashabiki na kuwasaidia kufanya mazoezi ili kuboresha afya zao.

Mashindano ya Sports Xtra Bonanza yalianzishwa miaka mitano iliyopita, ambapo shirika la fastjet limeshiriki mara zote na kufanikiwa kushinda vikombe vitano kwa kipindi chote hicho ikiwemo katika mechi za mikoani zilizochezwa katika mikoa ya Mwanza, Mbeya na Kilimanjaro. 

Mashindano haya yanaandaliwa na Clouds FM kupitia kipindi chake cha michezo cha Sports Xtra.