fastjet yawezesha madaktari kutoa huduma ya afya ya kinywa na meno Tarime

Na Bill Marwa / @BillMarwa

 

 

Madaktari kutoka chama cha madaktari wa kinywa na meno Tanzania walifanya ziara ya kujitolea katika wilaya ya Tarime mkoani mara ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya wiki ya afya ya kinywa na meno duniani ambapo walitoa huduma za uchunguzi, matibabu na elimu kwa wakazi wa wilaya hiyo ikiwa ni pamoja na kuwafikia wanafunzi na watoto yatima.

 

Akizungumza hivi karibuni wilayani Tarime, Daktari wa Meno wa  Wilaya ya Ngara mkoani Kagera, Dk. David Mapunda, alisema ziara hiyo imewapatia fursa madaktari hao kufanya uchunguzi wa  kinywa pamoja na kutoa huduma za matibabu pamoja na elimu kwa wakazi wa wilaya hiyo.

 

Alisema miongoni mwa magonjwa yanayosumbua katika kinywa ni pamoja na  kuoza kwa meno na ugonjwa wa fizi ambayo  yanasababishwa na uchafu unaotokana na kutokupiga mswaki, kukosea kupiga mswaki au kutumia mswaki usiofaa.

 

Alisema ili wananchi waepukane na magonjwa hayo ya meno wanapaswa kupiga mswaki angalau mara mbili kwa siku na kujenga utaratibu wa kuangalia afya ya kinywa na meno mara kwa mara.

 

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Kinywa na Meno wa Mkoa wa Mara, Dkt Nila Jackson, alisema kati ya Machi 13 hadi 16 mwaka huu madaktari hao walifikia jumla ya wananchi 710 katika kijiji cha Nyamwaga wakiwemo wanafunzi 510 kutoka shule za msingi saba kijijini humo.

 

"Kati ya tarehe hizo Madaktari hao walitoa uchunguzi, matibabu na elimu ya afya ya kinywa na meno na  kati ya tarehe 17 hadi 20 walikuwa katika wilaya ya Tarime na Rorya kuendelea na zoezi hilo," aliongeza Dk. Jackson

 

Naye Rais wa Chama cha Madaktari wa Kinywa na Meno Tanzania (Tanzania Dental Association), Dkt. Ambege Jack Mwakatobe, alitaja kauli mbiu ya mwaka huu ya siku ya kinywa na meno Duniani inayosema “Sema ah, fikiria kinywa, fikiria afya” ambayo inalenga kuwahamasisha wananchi kuzingatia afya ya kinywa na meno ili kujikinga na magonjwa yanayohusiana na ugonjwa wa meno ikiwemo magonjwa ya kisukari na mengine.

 

Aidha alitoa wito kwa madaktari wa mikoa kuendelea kutoa elimu kwa wananchi angalau mara mbili kwa mwezi ili kuwaongezea ufahamu na uelewa wananchi juu ya usafi wa kinywa.

 

Akizungumza kutoka kijiji cha Nyamwaga, Msemaji wa fastjet nchini, Lucy Mbogoro,  alisema shirika la fastjet linafuraha kuwa sehemu ya shughuli hii inayofanywa na madaktari hawa wazalendo.

 

"Shirika la fastjet limewawezesha madaktari hawa kusafiri kutoka Dar es salaam hadi Mwanza na kurudi kwa mwaka wan ne mfululizo, ikiwa ni sehemu ya mpango wake wa kurudisha shukrani kwa jamii," alisema.