RDJ Kwachee: Kiukweli sipendi kujiangalia kwenye luninga

Yawezekana umewahi kunisikia kama Jimmy Jam nilipokua nafanya kazi DTV, kwa sasa wengi wananifahamu kama RDJ Kwachee, jina langu halisi ni Jamal Abdallah, mtangazaji wa TV-E na redio EFM. Situmii kilevi. Napenda kuogelea, kuangalia filamu na kutembelea ndugu, jamaa na marafiki.

Safari ya utangazaji

Safari yangu ya utangazaji ilianza kama utani. Nilikua napenda sana muziki na kwa bahati nzuri nilikua nafahamiana na bosi wangu wa sasa Majay ambaye kwa wakati huo alikua mtangazaji wa redio Magic FM, nilikua nafuatana naye akienda kwenye kipindi. Baada ya muda aliacha kazi na kuanzisha kituo cha televisheni, nikahamia huko ambapo nilianza kufanya kazi kama mrusha vipindi. Baada ya muda televisheni ile ilifungwa na ndipo niliamua kufanya kazi ya UDJ kwenye sherehe mbalimbali kwa kipindi cha mwaka mmoja kati ya 2012 - 2013.

EFM ilipoanzishwa na Majay mwaka 2014, nilianza kazi kama DJ, kisha mtangazaji wa kipindi cha nyimbo za zamani za Bongo Fleva. Mnamo mwaka 2016 TV-E ilipoanzishwa, nikaanza kazi kama mkuu wa kitengo cha urushaji matangazo na baadaye mtangazaji wa kipindi cha Kwachee on the streets kinachorushwa mara tatu kwa wiki. Kitaaluma nimesomea mawasiliano ya umma chuo kikuu cha Tumaini.

 

Kwachee on the streets

Kwa kawaida kipindi kinahusisha uwepo wa mtu mashuhuri. Tunaingia mtaani na kuzungumza na wananchi kuhusu maswala ya kijamii. Watu wengi wanavutiwa kuwaona wanamuziki na wacheza filamu wanaowapenda. Kuna wakati tunajikuta tunafuatwa na kundi kubwa la watu kila tunapoenda.

Napenda kuwauliza watu maswali ya ufahamu lengo likiwa kuelimisha na kuburudisha. Mwishoni tunatoa majibu ya maswali yetu ili watu wote wafahamu majibu sahihi.

Kipindi cha Kwachee on the streets kinaruka siku za Jumatatu, Jumatano na Ijumaa na hurudiwa mara tatu kwa wiki.

 

Unajiskiaje kuangaliwa kwenye TV?

Kwanza sipendi kujiangalia kwenye luninga. Nafurahi kuona kipindi changu kinatazamwa na watu wengi barani Afrika. Wengi wanasema kipindi kinawavutia, kinawafundisha na kuwaburudisha pia. Naamini nafanya kitu cha tofauti na cha kibunifu. Wengi wananiambia wangependa kufanya kazi kama yangu. Mapokeo ni mazuri sana. Kwakweli siwezi kufananisha maisha yangu kabla ya kuwa mtangazaji na sasa, nimejenga mtandao mkubwa wa watu ninaofahamiana nao.

 

Ushauri kwa wanaopenda kuwa watangazaji

Naamini katika kufanya kazi kwa bidii. Kuamini katika kitu unachokipenda. Usikate tamaa, katika kujaribu kufikia ndoto zako haijalishi unakosea mara ngapi, amka na pambana tena. Watangazaji ni lazima wawe na benki ya maneno, wasome na watafiti juu ya mambo kabla ya kuyazungumzia.

 

Bill Marwa - @BillMarwa